DEAL PLUS

Karibu DEALPLUS BLOG uweze kupata habari za Michezo, Siasa, Afya na Burudani kutoka ndani na nje ya nchi.

Breaking


Wednesday, 11 August 2021

Mama wa Askari aliyepotea asimulia maisha yake


uchunguuupiccc

Mama mzazi wa polisi Emmanuel Govela, Monica Maluli

Mama mzazi wa kachero wa polisi aliyetoweka kwa takriban siku 45 amesimulia maisha ya mwanaye, Emmanuel Govela aliyelitumikia Jeshi la Polisi kwa miaka 19, kwamba alikuwa msiri.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na mama mzazi wa Emmanuel, Monica Maluli (61) kwenye mahojiano maalumu aliyofanya na gazeti hili kijijini kwake, Mtera mkoani Dodoma.

Monica anaishi umbali wa kilomita 103 kutoka Dodoma mjini, Kijiji cha Mtera, Wilaya ya Mpwapwa mahali ambapo kila mmoja anaonekana kupigwa butwaa kuhusu tukio la kutoweka kwa Inspekta Emmanuel Govela aliyekuwa akifanya kazi Kituo cha Polisi katika Mji wa Kiserikali, Mtumba jijini Dodoma.

Emmanuel ni mtoto wake wa kwanza kati ya watoto watano aliozaa na mumewe Yuda Govela aliyekuwa mfanyakazi wa Tanesco. Yuda alifariki duniani 2004.

Monica anasema mwanawe huyo alizaliwa wakati wa Krismasi, Desemba 25, 1982 saa 12 jioni katika eneo la Ilula mkoani Iringa na wakati wa utoto ndoto ya Emmanuel alitaka kuwa daktari wa binadamu.

Anasimulia kuwa Emmanuel aliyesoma Shule ya Msingi Mtera Dam na baadaye sekondari ya Mtera alikomaliza kidato cha nne mwaka 2000, alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 2002.



uchungupic

Emmanuel Govela

Monica anamuelezea mwanaye huyo kwamba tangu baba yake mzazi afariki dunia mwaka 2002, jukumu la kulea familia ikiwamo kuwasomesha wadogo zake wanne ambao wote wa kiume lilibebwa na kachero huyo wa polisi.

Anasema mwanawe alianzia kazi katika mkoa wa Manyara kabla ya mwisho wa mwaka jana kuhamishwa Dodoma ambako walipata taarifa kuwa amepewa ukuu wa kituo katika mji wa Serikali Mtumba.

Anaeleza kuwa, licha ya upenzi wa kurudi nyumbani (Mtera), mwanawe hana mapenzi ya kulala huko, bali huenda asubuhi na kuondoka nyakati za jioni.

“Upenzi wake mkubwa hata likizo huwa ni Dar es Salaam, ndiyo maana hata mwezi wa tano alisema atakuwa na likizo ya wiki tatu ambayo angeitumia huko ambako ana ndugu na marafiki pia,” alisema.

Soma zaidi:Ndugu walia askari polisi kutoweka siku 41

Monica ambaye wanaishi jirani na eneo uzalishaji umeme la bwawa la Mtera, anasema wao ni wenyeji wa Iringa, lakini mumewe alihamishiwa hapo kikazi akitokea Iringa na umauti ulikuta hapo, lakini kwa kuwa alijenga nyumba ya kuishi eneo hilo ndio wameendelea kuishi hadi sasa.

Nyumba hiyo imo ndani ya uzio wa bwawa la Mtera na iko jirani na geti kama umbali wa mita 30, nje ya nyumba hiyo kukiwa na mbuyu mkubwa, pande zote imepambwa kwa mandhari ya mawe.

Kuhusu mwanae kuoa

Monica anasema mara ya mwisho kuwasiliana na mwanae ilikuwa Mei mwaka huu ambapo alimueleza nia yake ya kutaka kuoa.

“Mwezi wa tano nilikuja mjini (Dodoma), niliongea naye mambo mengi lakini aliniambia ana mipango ya kuoa mwaka huu, lakini akasema asingefunga ndoa sababu anataka akae na mke amchunguze kwanza jambo ambao nilimkubalia,” amesema Monica huku akifuta machozi.

Soma zaidi:Polisi wafunguka ofisa wake aliyepotea

Maisha yao

Monica anasema mumewe alihamishiwa Mtera akitokea mkoani Iringa alipokuwa fundi umeme na ndipo wakaanzisha mji mwingine wakati huo Emmanuel akiwa ni mdogo, hivyo safari ya elimu alianzia hapo.

Anasema katika maisha yake mwanawe amekuwa na huruma na wadogo zake hata ikawa chanzo cha kuchelewa kwake kuoa ili amalize jukumu la wadogo zake walau nao waanze kujitegemea.

“Mmoja ndiyo huyo Humphrey ambaye anamaliza UDOM mwaka huu, mwingine mtendaji huko Babati na wengine alishawasaidia wanajitegemea, nalia sijui chozi litakwisha lini,” anasema.

Miongoni mwa sifa anazompa kijana wake ni upole na umakini katika kupanga mipango yake na kwamba alijaliwa kuwa msiri tangu utoto, hivyo mipango mingi aliyopanga haijulikani na ndiyo maana hakumweleza mama yake anamuona nani na wa wapi.

Mawasiliano yapotea

Monica anasema mdogo wa Emmanuel ambaye anasoma UDOM alianza kulalamika kuwa hampati kaka yake kwenye simu ambayo si kawaida yake, jambo lililoamsha hofu na wengine waanze kumtafuta.

Hata hivyo, hali hiyo haikusaidia hadi mdogo wake (Athuman) aliposafiri kutoka Manyara hadi Dodoma ili akajue ukweli wa jambo hilo ndipo ikabainika kuwa hayupo kazini.

“Walikwenda Mtumba ambacho ndiyo kituo chake, hawakumuona lakini cha ajabu hapo waliambiwa alikuwa na siku 29 hawamuoni eti nao walikuwa wanamtafuta, basi wanangu Athuman na Humphrey waliongozana na rafiki wa Emma anaitwa Ulimboka wakaenda alikokuwa anaishi,” anaeleza.

Wakiwa huko walikuta chumba kimefungwa na kwa msaada polisi na mwenye nyumba walivunja mlango ambako walikuta vitambulisho vya kazini, kadi ya benki, simu, sare za polisi na vitu vingine jambo lililoongeza mashaka.

Hofu ya Mama

Anasema tumaini la kumpata mwanawe linatoweka kutokana na kauli aliyoambiwa yeye mwenyewe alipokwenda polisi ambapo wakimweleza kuwa wanapata ugumu kumtafuta, hivyo wakaitaka familia itumie mbinu zozote kumtafuta.

Anasema ukoo wa Govela wa Iringa wamegawana majukumu ya kumtafuta ndugu huyo bila mafanikio alichobakiza ni chozi lake ambalo halitakauka.

Huku akifuta machozi anasema, “namuomba mwanamke mwenzangu Rais Samia (Samia Suluhu Hassan) aingilie kati jambo hili mwanangu apatikane akiwa hai, lakini kama amekufa basi nionyeshwe maiti yake au kaburi lake,” anasema Monica.

Hata hivyo, anasema ndugu walioko Ilula bado wanaendelea kuhangaika kwa kutafuta kila kona ya nchi baada ya kuona kauli ya polisi kama inawavunja moyo.

Chozi halitakauka

Monica anasema furaha aliyoipa Krismasi ya mwaka 1982 imezimwa ghafla, lakini bado ataendelea kumlilia Mungu akisema iko siku Mungu ataonyesha miujiza yake.

“Sisi ni Wahehe, kila mmoja analia kivyake na kwa kweli machozi yangu...hayataenda bure acha niishi hivi ilivyoamuliwa,” alisema.

Kwa mujibu wa mama huyo, kila wakati amekuwa akisafiri kwenda Ilula ambako ndani ya muda mfupi ameamua kuuza mali zake yakiwemo na mashamba ya Emmanuel ili apate fedha za kuzunguka.



No comments: