MKUU wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amekasirishwa na kuendelea kwa migogoro ya wakulima na wafugaji licha ya kuwa na sheria za kukabili migogoro hiyo hali inayofanya viongozi kutumia muda mwingi kusuluhisha na kuacha kufanya shughuli za maendeleo.

Kunenge ameyasema hayo mjini Kibaha wakati wa mkutano wa mashauriano kuhusu Mpango wa kukabiliana na migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi kwa kutumia mfumo wa ranchi ndogo kwenye mkoa huo.

Amesema migogoro hiyo iishe na ibaki historia na mkoa hauwezi kuwafumbia macho watendaji na wataalam ambao wataonekana kuwa wanashiriki kwenye migogoro hiyo ambayo imesababisha viongozi kutofanya shughuli nyingine na kubaki kusuluhisha migogoro hiyo.

Naye mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainab Abdala amesema kuwa migogoro hiyo ni kero kubwa sana ambapo wakati wanaitatua wanapigiwa simu na baadhi ya vigogo.

Abdala amesema wafugaji hao wamekuwa wakitumika na baadhi ya watu wenye uwezo ambao ndiyo wanaowakingia kifua na kusababisha wafugaji kukosa haki zao.

Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete amesema  changamoto kubwa ni wafugaji wavamizi kuingia kwenye maeneo bila ya kufuata sheria.