Kocha wa Chelsea ageuka mnyama
Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte amesema yeye huwa "mnyama" wakati wa mechi, baada yake kushuhudia viongozi hao wa Ligi ya England wakilaza Everton 3-0 Jumapili.
Mwitaliano huyo alisherehekea uwanjani na wachezaji wake baada ya mchezo kumalizika Goodison Park, ambapo mabao yalifungwa na Pedro, Gary Cahill na Willian.
Chelsea wanahitaji kushinda mechi tatu kati ya nne walizosalia nazo msimu huu kushinda taji la ligi, msimu wa kwanza chini ya Conte.
"Kuna Antonio wawili. Ni watu wawili tofauti," alisema Conte, 47.
"Wakati wa mechi, najua kwamba mimi huwa mnyama.
"Baada ya mechi, lazima niwe nimetulia baada yetu kushinda lakini nafikiri ni vyema kusherehekea (ushindi) na wachezaji, wafanyakazi na mashabiki. Hili lina maana kubwa katika maisha yangu."
Conte, ambaye alishinda mataji matatu mtawalia ya ligi ya Serie A akiwa na Juventus kati ya 2012 na 2014, anafahamika sana kwa vituko vyake na nguvu anazoonekana kuwa nazo akielekeza mechi inapokuwa inaendelea.
Alisherehekea mabao ya klabu yake dhidi ya Everton kwa kuruka na kurusha ngumi hewani na kukimbia sehemu inayotengewa wakufunzi nje ya uwanja.
Mwitaliano huyo huwa ametulia wakati wa mahojiano na wanahabari kabla na baada ya mechi, sifa ambazo anasema huwa anapenda wachezaji wake wawe nazo.
"Lazima tuwe na furaha kwa sababu tulicheza mchezo kwa kutumia vichwa vyetu, na kipindi kama hiki katika msimu, ni muhimu kutumia vichwa vyetu, kisha moyo na baadaye miguu," alisema.
Conte anaamini sana kuhusu hilo, kiasi kwamba aliandika kitabu chenye kichwa Testa, cuore e gambe (Kichwa, moyo na miguu) mwaka 2014.
Mechi za Chelsea zilizosalia 2016-17
Jumatatu, 8 MeiMiddlesbrough (Nyumbani)
Ijumaa, 12 MeiWest Brom (Ugenini)
Jumatatu, 15 MeiWatford (Nyumbani)
Jumapili, 21 MeiSunderland (Nyumbani)
Jumamosi, 27 MeiArsenal (fainali Kombe la FA)
No comments:
Post a Comment