DEAL PLUS

Karibu DEALPLUS BLOG uweze kupata habari za Michezo, Siasa, Afya na Burudani kutoka ndani na nje ya nchi.

Breaking


Thursday 27 July 2017

FAHAMU KUHUSU SARATANI YA KIBOFU CHA MKOJO


Kibofu cha mkojo kinapatkana sehemu ya chini ya maeneo ya tumbo na ni kiungo ambacho kina uwazi/tundu ndani yake na kazi yake kubwa ni kukusanya na kuhifadhi mkojo unaotolewa na figo kabla ya kuutoa nje ya mwili wa binadamu. Kibofu cha mkojo kina kuta (layers) aina tatu za tishu ambazo ni;-

1.Mucosa layer – Kuta ya ndani kabisa ambayo ndio inayokutana na mkojo wa binadamu. Kuta hii nayo inakuta nyingi sana za seli au chembechembe zinazojulikana kama transitional epithelium cells ambazo pia hupatikana kwenye sehemu ya mirija inayojulikana kama ureters, urethra na kwenye figo. Seli hizi zinazuia uvujaji wa mkojo kwenda kwenye sehemu nyengine ya mwili.
Ureter huingiza mkojo kutoka kwenye figo na urethra hutoa mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kukojoa.

2.Lamina propia – Kuta ya katikati nyembamba sana kati ya kuta hizi tatu na  ambayo mishipa ya damu na neva inapatikana hapa na ni muhimu sana wakati wa kupanga makundi ya saratani ya kibofu cha mkojo wakati wa tiba.

3.Muscularis layer - Kuta ya nje ambayo ndani yake kuna destrusor muscle na ndio kuta nene kati ya hizi tatu. Kazi yake kubwa ni kupumzisha kibofu cha mkojo ili mkojo uingie ndani na ukishajaa basi hukaza kibofu (contracts) na kufanya mkojo kutoka nje.
Nje ya hizi kuta tatu, kibofu cha mkojo kimezungukwa na mafuta ambayo hukinga kibofu kutokana na mtikisiko wowote na kukitenganisha na viungo vengine. Kuna saratani aina tatu kutokana na kuta hizi tatu nilizotaja hapo juu za kibofu cha mkojo
Urothelial carcinoma (transitional cell carcinoma) – Hii ndio aina ya saratani inayotokea kwa wingi na hutokea kwenye seli za transitional epithelium cells. Asilimia 90 – 95 ya saratani zote za kibofu cha mkojo huwa ni aina hii.
Squamous cell carcinoma – Aina hii hutokea baada ya maradhi ya kwenye kibofu cha mkojo kwa muda mrefu kama vijiwe vya kibofu cha mkojo (bladder stones) na huchukua asilimia 1- 2 ya saratani zote za kibofu cha mkojo. Huonekana sana maeneo ya mashariki ya kati na afrika. Aina hii ina uhusiano mkubwa na ugonjwa wa kichocho (schistosomiasis) cha muda mrefu.
Adenocarcinoma – Hutokea baada ya inflammation ya kwenye kibofu cha mkojo kwa muda mrefu. Na huchukua asilimia 2 ya saratani zote za kibofu cha mkojo.

VIHATARISHI VYA SARATANI YA KIBOFU CHA MKOJO
Wale wanaofanyakazi kwenye saluni za nywele
Wanaofanya kazi ya kupaka rangi
Wafanyakazi wa viwanda vya nguo
Wanaofanya kazi kwenye viwanda vya ngozi
Wafanyakazi wa viwanda vya mipira (rubber)

Uvutaji sigara – Wavutaji sigara wako kwenye hatari ya kupata saratani hii mara mbili zaidi ya wale wasiovuta sigara.
Asili ya mtu – Saratani hii huonekana zaidi kwa watu weupe kuliko watu weusi. Watu wa mashariki ya kati wanaasilimia ndogo zaidi.

Umri – Huonekana zaidi kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 40 lakini huweza kutokea kwenye umri wowote ule.
Jinsia – Hutokea sana kwa wanaume mara mbili au tatu zaidi kuliko kwa wanawake

Lishe – Watu wanaokula kwa wingi nyama za kukaanga kwa mafuta na kutumia mafuta yatokanayo na wanyama wakati wa kupika wako kwenye hatari kubwa kupata saratani hii. Aristolochia fangchi ni mti wa mitishamba unaotumiwa na watu wa jamii ya Wachina katika kupunguza uzito kwa wale wenye uzito uliopitiliza na hata kwenye baadhi ya dawa za kichina, watu wanaotumia mti huu au dawa inayotokana nao pia wako kwenye hatari kubwa sana kupata saratani hii.

Historia ya matumizi ya dawa za saratani kama za saratani ya matiti nk.
Historia ya saratani ya kibofu cha mkojo kwenye familia. Inahusishwa na mabadiliko katika viashiria vya asili au jena (genes) aina ya HRAS, KRAS2, RB1, FGFR3.
Madereva wa malori (truck drivers) – Pia wako kwenye hatari kubwa
Baadhi ya kemikali zinauhusiano na saratani ya kibofu cha mkojo kama
DALILI NA VIASHIRIA VYA SARATANI YA KIBOFU CHA MKOJO
Kukojoa damu (gross haematuria) ambayo inaweza kuonekana kwa macho au kwa hadubini (microscopic haematuria)
Maumivu wakati wa kukojoa au kichomi wakati wa kukojoa (burning sensation)
Kukojoa mara kwa mara (frequency of urination)
Maumivu nyuma ya mgongo
Kuhisi bado mtu hajamaliza mkojo baada ya kukojoa awali
Kuhisi mkojo ambao hautoki
Kushindwa kujizuia kukojoa baada ya kukojoa awali (urgency)
Uvimbe wa saratani ndani ya kibofu cha mkojo
Dalili na viashiria vengine ni
Maumivu ya tumbo
Upungufu wa damu mwilini
Uzito kupungua
Maumivu ya mifupa
Kujikojolea
BAADHI YA DALILI NA VIASHIRIA HIVI VINAWEZA KUONEKANA KWA WAGONJWA WA SARATANI YA FIGO, TEZI DUME NA CYSTITIS.
Vipimo vya uchunguzi
Cystoscopy – Mpira unaoingiziwa kwenye mrija wa wa kutolea mkojo ambao una kamera mbele na taa ili kuchunguza kama kuna uvimbe wa saratani ya kibofu cha mkojo na kuchukua nyama kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara zaidi
Biopsy – Nyama iliyochukuliwa kwa kipimo hapo juu, huchunguzwa kwenye maabara ili kuthibitisha kama ni saratani
Ultrasound ya tumbo na nyonga – Kuangalia kama kuna uvimbe kwenye kibofu cha mkojo au kwenye figo. Inaweza kugundua sababu nyengine ya kukojoa damu kama vijiwe kwenye kibofu cha mkojo (bladder stones) au uvimbe kwenye tezi dume (prostate enlargement).
Kipimo cha mkojo (Urinalysis) – Kinaweza pia kugundua sababu ya kukojoa damu na kama kuna ugonjwa mwengine wowote wa kibofu cha mkojo
Kipimo cha damu (Complete blood count) – Kuangalia wingi wa damu, kundi la damu iwapo mgonjwa atahitaji kuwekewa damu nk.
CT scan na MRI – Husaidia katika uchunguzi wa saratani kwani hutoa maelezo mazuri na pia huweza kugundua saratani kama ipo kwenye figo, nyonga na sehemu nyengine mwilini.
Pyelography – Hii ni aina ya x-ray ya kibofu cha mkojo ambayo hupigwa mgonjwa baada ya kuchomwa dawa maalum (contrast dye) kwenye mishipa ya damu (Intravenous pyelography) au kwenye mrija wa kutoa mkojo (urethtra) na hujulikana kama retrograde pyelography.
Bone scan – Kuangalia kama saratani imesambaa hadi kwenye mifupa
Picha ya kifua (Chest X-ray) – Kuangalia kama saratani imefika kwenye mapafu.

MAKUNDI YA SARATANI YA KIBOFU CHA MKOJO
Kabla ya mgonjwa kupewa tiba, ni muhimu kwa daktari kwanza kujitahidi kujua kundi (stage) la saratani aliyonayo mgonjwa. Saratani hii imepangwa katika makundi tofauti kulingana na kama inaweza kutibiwa kwa njia ya upasuaji, kama imeenea hadi kwenye tezi (lymph nodes) na kama saratani imesambaa kwenye sehemu nyengine mwilini.

UMUHIMU WA KUPANGA MAKUNDI YA SARATANI
Inasaidia kuchagua tiba sahihi ya saratani ya mgonjwa
Saratani iliyo ndani sana inauwezekano mkubwa wa kusambaa kwenye tezi na sehemu nyengine mwilini kuliko ile ambayo ipo juu.
Kadri namba ya kundi inapoongezeka ndio ugonjwa ulivyo mbaya zaidi na asilimia ya kuishi kwa muda mrefu hupungua.
Husaidia katika kuwapanga wagonjwa kwenye makundi na hivyo basi kuweza kuwafanyia utafiti kutumia matibabu mapya kwa urahisi zaidi.
Makundi ya saratani ya kibofu cha mkojo ni kama yafuatavyo
STAGE 0 – SELI ZA SARATANI ZINAPATIKANA KWENYE KUTA YA NDANI YA KIBOFU CHA MKOJO TU

STAGE I – SELI ZA SARATANI ZIMEENEA KUTOKA KWENYE KUTA YA NDANI YA KIBOFU CHA MKOJO LAKINI HAZIJAFIKA KWENYE NYAMA (MUSCLES) YA KIBOFU CHA MKOJO

STAGE II – SELI ZA SARATANI ZIMEFIKA KWENYE NYAMA ZA KIBOFU CHA MKOJO LAKINI HAZIJAFIKA KWENYE TISHU ZA MAFUTA ZILIZOZUNGUKA KIBOFU CHA MKOJO.

STAGE III – SELI ZA SARATANI ZIMEFIKA KWENYE TISHU ZA MAFUTA ZINAZOZUNGUKA KIBOFU CHA MKOJO HADI KWENYE TUPU YA MWANAMKE (VAGINA), TEZI DUME (PROSTATE), MFUKO WA UZAZI (UTERUS) LAKINI HAZIJAFIKA KWENYE TEZI (LYMPH NODES) AU KWENYE VIUNGO VENGINE MWILINI.

SSTAGE IV – SELI ZA SARATANI ZIMEFIKA KWENYE TEZI, NYONGA, KUTA ZA TUMBO (ABDOMINAL WALL) NA VIUNGO VENGINE MWILINI.
RECURRENT – SARATANI IMEJIRUDIA KWENYE KIBOFU CHA MKOJO AU KWENYE VIUNGO VENGINE BAADA YA KUTIBIWA HAPO AWALI.Saratani ya kibofu cha mkojo inakawaida ya kusambaa kwenye tezi, na kupitia kwenye damu hadi kwenye mapafu, ini, mifupa na sehemu nyengine za mwili

TIBA YA SARATANI YA KIBOFU CHA MKOJO
Saratani hii ni kati ya saratani zinazojulikana kuwa na asilimia kubwa ya kujirudia baada ya kutibiwa.Saratani ya kibofu cha mkojo ina uwezekano mkubwa wa kutibika kama itagundulika mapema. Tiba hutegemea ;na aina ya saratani
Kundi la saratani (stage)
Historia ya kutibiwa saratani yoyote hapo awali
Umri wa mgonjwa
Afya ya mgonjwa (ili kuweza kujua kama mgonjwa atahimili aina ya tiba, kuna wagonjwa wengine huwa wanakuwa wamedhoofika sana).
Tiba imegawanyika kwenye
Tiba ya mionzi
Tiba ya dawa
Tiba ya upasuaji
Tiba ya immunotherapy ama biological therapy
Tiba ya mionzi (Radiation therapy)
Mionzi hutumika kuua seli za saratani. Tatizo la tiba hii ni kwamba inaua seli za saratani pamoja na seli za kawaida na hutumika kama njia mbadala ya tiba ya upasuaji. Matumizi yake ni kwenye saratani ndogo zilizoathiri nyama ya kibofu cha mkojo. Tiba hii ipo ya aina mbili;
Mionzi inayotolewa kwa kutumia mashine ya mionzi (external radiation)
Mionzi inayotolewa kwa kupachika kifaa cha kutolea mionzi ndani ya mwili kwa kukiingiza kupitia kwenye mrija wa kutoa mkojo (urethra) au kupitia upasuaji mdogo kwenye maeneo ya kibofu cha mkojo na kukiweka kifaa hicho ndani ya kibofu cha mkojo (Internal radiation).

MADHARA YA TIBA YA MIONZI NI KAMA YAFUATAYO
Kujisikia uchovu au kuchoka
Kichefuchefu
Sehemu ya ngozi ambayo mionzi imepita kuwa kavu,nyeusi au nyekundu na kuwasha
Matatizo ya mkojo
Kupata maradhi kirahisi kwa kuwa inapunguza kinga mwilini
Upungufu wa damu mwilini (anaemia)
Tupu kuwa kavu kwa wanawake (vaginal dryness)
Kwa wanaume - Uume au dhakari kushindwa kusimama au kusimika (impotence)
TIBA YA DAWA (CHEMOTHERAPY)
Tiba hii inaweza kutumika pekee au pamoja na tiba ya upasuaji au ya mionzi au kutumika pamoja na tiba ya upasuaji na mionzi (kutumika dawa + upasuaji + mionzi). Pia inaweza kutumika kabla ua baada ya tiba nyengine. Dawa za saratani ya kibofu cha mkojo ni Methotrexate (M), Vinblastine (V), Doxorubicin (A) Cisplastin (C) au MVAC. Kwa wale wenya matatizo ya moyo hupewa CMV.
Dawa zinaweza kutumiwa kwa wale wenye saratani iliyosambaa mwilini au wale ambao wapo kwenye makundi kuanzia Stage 0 hadi Stage III baada ya upasuaji ili kupunguza uwezekano wa kujirudia na tiba hii hujulikana kama adjuvant chemotherapy.
Pia dawa hizi zinaweza kutolewa kabla ya upasuaji ili kuongeza ufanisi wa upasuaji na kupunguza ukubwa wa uvimbe wa saratani na tiba aina hii hujulikana kama neoadjuvant chemotherapy.
Wagonjwa wa Stage 0 na Stage I wanaweza kupewa dawa kupitia mpira unaojulikana kama catheter na dawa hukaa kwa muda (masaa kadhaa) na hutolewa baadae kwa njia ya kukojoa, hii hufanyika mara moja kwa wiki na huendelea kwa muda wa wiki kadhaa.
MADHARA YA TIBA HII NI PAMOJA NA
Kuchoka
Kichefuchefu
Kutapika
Nywele kunyofoka
Kupungikiwa na damu mwilini
Kupungua hamu ya kula
Madhara hutofautiana kati ya mgonjwa mmoja na mwengine.
Kibofu cha mkojo kwenye maumbile ya mwanamume
TIBA YA UPASUAJI
Kuna aina tatu za upasuaji;
Transurethral resection with fuguration – Aina hii inahusisha kuondoa uvimbe wa saratani kutoka kwenye kibofu cha mkojo na hutumiwa kwa wagonjwa wa Stage 0 na Stage I na baada ya upasuaji hupewa dawa za saratani.
Radical cystectomy – Inahusisha uondoaji wa kibofu chote cha mkojo, tezi pamoja na viungo vengine vya mwili kwa wale ambao saratani imeenea hadi kwenye nyama za kibofu cha mkojo au saratani ambayo haijaingia ndani lakini haipungui au kuleta matokeo 
MADHARA YA SARATANI YA  KIBOFU CHA MKOJO
Upungufu wa damu mwilini
Kushindwa kuzuia mkojo na hivyo kujikojolea
Kupungua kwa tundu kwenye mrija wa kutolea mkojo (urethral stricture)
Kuvimba kwa ureters kutokana na mkojo kushindwa kwenda kwenye kibofu cha mkojo
KINGA YA SARATANI YA KIBOFU CHA MKOJO
Acha kuvuta sigara
Kunywa maji kwa wingi anagalau lita 1 na nusu kwa siku ili kusaidia kuondoa kemikali zinazosababisha saratani mwilini. ‘’Kumbuka kunywa maji mpaka wakati unapokojoa mkojo unatoka bila rangi yoyote’’.
Kwa wale wanaofanya kazi viwandani, saluni, nk, hakikisha unajikinga kutokana na madhara ya kemikali zinazosababisha saratani.