Mkurugenzi wa bodi ya TBS, Dkt. Eliapenda Mariki akifungua warsha ya wadau kuhusu ushiriki katika uandaaji wa viwango iliyofanyika mapema jana Mkoani Morogoro. Baadhi ya washiriki wa warsha ya ushirikishwaji wa wadau katika uaandaji Viwango iliyofanyika mapema jana mkoani Morogoro
**************************
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) na wadau katika uandaaji wa viwango wameshauriwa kuongeza juhudi za kuoanisha viwango katika ngazi za kikanda na kushriki kikamilifu katika michakato wa kutayarisha viwango vya kimataifa ili kuziwezesha bidhaa kupenya kwenye masoko ya kimataifa.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS, Dkt.Eliapenda Mariki, wakati akifungua warsha ya ushirikishwaji wa wadau katika uandaaji wa viwango nchini.
Warsha hiyo iliyofanyika mkoani Morogoro ilienda sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani Kwa mwaka 2022.
Dkt. Mariki alisema viwango vina mchango katika juhudi za dunia katika kufikia malengo endelevu (SDGs) kwani hutoa suluhisho halisi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Dkt. Mariki alisema mojawapo ya sababu zinazofanya bidhaa za nchi zinazoendela ikiwemo Tanzania kushindwa kupenya na kuingia kwenye masoko ya kimataifa ni kushindwa kwa bidhaa hizo kukidhi matakwa ya viwango.
"Wakati mwingine bidhaa hushindwa kuingia kwenye soko la kimataifa au la kikanda kutokana na tofauti za masuala ya matakwa ya kiwango cha bidhaa husika baina ya nchi na nchi na hatimaye" alisema Dkt. Mariki na kuongeza;
"Kwa sababu hii ni dhahiri kuwa iwapo kutakuwa na uoanishaji wa matakwa ya ubora baina ya nchi na nchi na hatimaye kuwa na viwango sawa kikanda na kimataifa, uwanja wa biashara utakuwa umesawazishwa."
Alifafanua kuwa viwango vina mchango mkubwa katika juhudi za dunia za kufikia malengo endelevu ya agenda 2030, kwani hutoa suluhisho halisi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Aliipongeza TBS kwa hatua ya kuwakutanisha wadau ili kuzungumza nao kuhusiana na ushiriki katika uandaaji wa viwango.
"Hii ni hatua muhimu katika msingi wa ushiriki wenye manufaa katika uandaaji wa viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa manufaa ya nchi," alisema Dkt. Mariki.
Madhimisho hayo yalianza kufanyika nchini kuanzia Oktoba 22, mwaka huu kwa shughuli mbalimbali za kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kushiriki mchakato wa uandaaji viwango kitaifa, kikanda na kimataifa.
Alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilibeba ujumbe usemayo;
" Viwango kwa Maendeleo Endelevu." Kwa mujibu wa Dkt. Mariki kauli mbiu hiyo inaendana na malengo ya maendeleo endelevu ambayo yanalenga kuweka usawa kijamii, kujenga uchumi endelevu na kupunguza kasi ya mabadliko ya tabia nchi.
No comments:
Post a Comment