DEAL PLUS

Karibu DEALPLUS BLOG uweze kupata habari za Michezo, Siasa, Afya na Burudani kutoka ndani na nje ya nchi.

Breaking


Monday 20 September 2021

TAHADHARI YATOLEWA KWA WANAONUNUA VITU HIVI KUTOKA NCHI ZA NJE

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, amewataka Watanzania kutunza mazingira kwa kununua bidhaa rafiki zisizokuwa na kemikali zitokanazo na gesi haribifu zinazoweza kumong’onyoa tabaka la ozoni.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo
Jafo alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuhifadhi Tabaka la Ozoni.
Katika maadhimisho hayo Waziri Jafo, alifanya ziara ya kukagua maduka ya bidhaa za mitumba za viyoyozi na majokofu yanayotumia gesi haribifu na kusababisha kuharibu tabaka hilo.

Katika ziara hiyo alitoa elimu kwa mafundi mchundo wanaojihusisha na uuzaji na utengenezaji wa bidhaa za mitumba ya majokofu pamoja na viyoyozi vinavyotumia gesi.
Alisema ozoni ni tabaka la hewa ambalo liko katika anga la juu la pili linalofahamika kitaalamu kama stratosphere ambalo linaweka aina ya tabaka ama tambara angani na kuzuia mionzi mikali ya jua inayoweza kuleta athari katika afya za binadamu na viumbe hai kuja moja kwa moja duniani.

Alisema uharibifu wa tabaka la ozoni unasababisha madhara mbalimbali duniani ikiwamo kuongezeka kwa kiwango cha joto pamoja na kuleta mabadiliko ya tabia ya nchi jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu na viumbe hai.
"Wafanyabishara wengi wamekuwa wakiuza majokofu ya mtumba yanayotumia gesi R22 na kuharibu mazingira… uzeni mitungi ya gesi kuanzia R200 na kuendelea," alisisitiza.

Alitoa wito kwa vijana wanaojishughulisha na masuala ya ufundi wa viyoyozi na majokofu ya mtumba kutumia aina ya gesi inayoruhusiwa na viwango vya kimataifa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Mwema, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, alisema Dodoma inakuwa kwa kasi na kwamba kuna haja ya kutengeneza jukwaa la pamoja litakalosaidia kutoa elimu kwa wananchi.
“Ni kweli wananchi wamekuwa wakinunua majokofu ya mtumba ambayo yameonekana kuwa na madhara na hiyo yote inatokana na kutokuwa na uelewa juu ya madhara hayo, lakini sasa kama tutakuwa na jukwaa la pamoja la kutoa elimu juu ya madhara ya bidhaa hizi za mtumba nina imani bidhaa hizo za mtumba hazitanunuliwa,” alisisitiza Mwema.
Mmoja wa mafundi anayejishughulisha na ufundi wa viyoyozi vya mtumba, Matukuta Juma, alisema kutokana na ushauri huo watahamasisha wengine kutumia mitungi ya gesi inayokubalika na kuiomba serikali kuwapunguzia bei gesi ambayo haiharibu mazingira.



No comments: