Na.Amon Mtega,Ruvuma.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma ya  Nishati na Maji Tanzania (EWURA) imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Tanesco  wa mkoa wa Ruvuma ili yawasaidie kufanya kazi kwa weledi zaidi pamoja na kujenga uelewa wa pamoja.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo mwakilishi wa mkurugenzi mkuu wa Ewura Titus Kaguo amesema  kumekuwepo na baadhi ya wafanyakazi wa Tanesco kutokuzingatia taratibu za utendaji kazi jambo ambalo limekuwa likisababisha madhara katika utoaji wa huduma za umeme.

Kaguo ambaye pia ni meneja mawasiliano wa Ewura amesema  kufuatia mafunzo hayo kwa wafanyakazi wa shirika la Tanesco yatawafanya waweze kubadilika na kufanya kazi kwa weledi zaidi ikiwemo na kuwatambua wakandarasi au mawakala  wenye leseni za Ewura wanaostahili kutoa huduma za wayaringi kwenye Nyumba za watu na kuwabana wale ambao hawastahili .

Baadhi ya Wafanyakazi wa Tanesco mkoa wa Ruvuma wakifuatilia kwa umakini maelekezo mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa kwenye mafunzo hayo.

Amesema kumekuwepo kwa baadhi ya hasara zilizokuwa zikitokea ikiwemo kuwaka majumba moto kwa sababu ya kutumia mafundi ambao hawana leseni za utambulisho wa kazi hizo.

Aidha amesema kuwa licha ya kuwapatia mafunzo haya kwa wafanyakazi wa Tanesco mkoani Ruvuma lakini Ewura itatoa mafunzo pia kwa mawakala wa Tanesco wanaotoa huduma za wayaringi kwenye majengo mbalimbali ya Serikali na Wananchi ili waweze kufuata taratibu.

Meneja wa Tanesco mkoa wa Ruvuma mhandisi, Florence Mwakasege akilalamikia kuwepo kwa baadhi ya mawakala ,wakandarasi ambao hawafuati taratibu.


Kwa upande wake meneja wa Tanesco mkoa wa Ruvuma mhandisi Florence Mwakasege ameipongeza Ewura kwa kutoa mafunzo hayo kwa wafanyakazi wa Tanesco ili kujenga uelewa wa pamoja.

Meneja Mwakasege pia ameeleza changamoto ambazo ofisi yake inakutana nazo kwa baadhi ya mawakala kugonga mihuri kwenye fomu za wateja wanaotakiwa kuingiziwa umeme bila hata kwenda kuangalia mazingira ya nyumba hizo jambo ambalo limekuwa likiibua migogoro baina ya wateja na ofisi ya Tanesco pindi mtafiti anapoona kuna makosa kwenye nyumba hizo.