Mtoto mwenye umri wa miaka ( 3) aliyejulikana kwa jina la Agness Charles mkazi wa wilaya ya Meatu Mkoa Simiyu amefariki dunia baada ya kudondokewa na matofali ya nyumba yao.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu Kamishna Msaidizi Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa limetokea septemba 29 mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku katika kijiji cha Mwanzangamba kata ya Mwanyahina Tarafa ya Kimali Wilayani Meatu.

Abwao amesema kuwa tukio hilo limetukia kufuatia tembo wawili kubomoa nyumba aliyolala mtoto huyo wakati wakiwa wanatafuta chakula aina ya viazi vikavu maarufu kama "michembe" baada ya kugundua kuwa ndani ya nyumba hiyo kuna chakula wanachohitaji.

Amesema mama mtoto huyo alikuwa wa kwanza kumuokoa na kumpeleka hospitali ya wilaya ya Meatu mara baada ya tembo hao kuondoka hata hivyo walikuta tayari ameshafariki.

Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari katika hospitali ya wilaya ya Meatu na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linatoa wito kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi kuendelea kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalam ili kudhibiti tembo kuingia vijijini.